19th Ave New York, NY 95822, USA

Papa dhidi ya Wakatholiki nchini Kenya

By Jacqueline Wahome| August 23, 2021

Maelezo ya Mhariri

Mwezi wa Machi mwaka huu Daktari Stephen Karanja kiongozi wa Chama cha Madaktari Wakatholiki nchini Kenya, aliandika waraka mrefu (na kwa sehemu nyingine wa kuchanganya) akishauri dhidi ya utumizi wa chanjo humu nchini; waraka huu ulimtaja mwanabiashara wa ulingo wa kiteknolojia Bill Gates na kudokeza  maslahi ya kivyama. 

Ushauri wake ulitofautiana na misimamo ya Chama cha Kimatibabu cha Katholiki na jumbe kutoka mji wa Vatican. Vile vile ilipendekeza kutumiwa kwa njia ambazo zimesemekana kuwa za uwongo za matibabu kama dawa ya hydroxychloroquine na mvuke. Miezi miwili baada ya kuchapisha kwa waraka wake Daktari Karanja ameunga orodha ya wanaokataa chanjo waliofariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19. 

Unapofikiria kundi la watu wanaopinga au kukataa chanjo wahudumu wa afya sio kati ya watu unaoweza kudhani wapo katika kundi hilo. Hata hivyo ugonjwa wa Corona umeonyesha kusuasua kwa kupashwa chanjo kwa wahudumu wa afya. Kwanza Chama cha Madaktari wakatholiki (KCDA) kilijitokeza na kupinga vikali kutumiwa kwa chanjo kupitia kwa barua ya wazi iliyochapishwa tarehe tatu mwezi wa Machi mwaka wa elfu mbili na ishirini na moja. Kanisa la Katholiki lilijitenga na ujumbe wa Chama hicho, ikitoa taarifa kwamba ni sawa na inakubalika kimaadili kupashwa chanjo zote dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 amabazo wizara ya afya inasema zinakubalika kimatibabu kuwa salama na zenye ufanisi. Chama cha KCDA kimeendelea kampeini zake dhidi ya kupashwa chanjo mpaka hii leo. 

Miezi mitatu baada ya nchi ya Kenya kupata chanjo zake za kwanza dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, data iliyopeanwa na wizara ya afya inaonyesha zaidi ya watu mia tisa na sabini elfu wamepata dozi yao ya kwanza. Nakufikia tarehe mbili mwezi wa Juni watu mia nne na sabini na moja wamepata dozi yao ya pili. Kati ya hawa ni wale walioorodeshwa kama watu wa kipaumbele kwenye zoezi hili na serikali. Orodha hiyo ikiwa na: wahudumu wa afya, walinzi, walimu na wengineo haswa wazee wenye miaka hamsini na nane na zaidi. 

Wahudumu wengine wa afya amabao ushauri wao tunauzingatia wana kusuasua kwa kupashwa chanjo ilhali wananchi wa kawaida wasio kwenye orodha iliyopewa kipaumbele wanasubiri fursa yoyote ya kupashwa chanjo hizo. Takwimu kutoka kwa wizara ya afya inaonyesha kuwa idadi za waliopashwa chanjo kati ya wahudumu wa afya ziko chini. 

Tangu tarehe saba mwezi wa Aprili data ya hapo awali ambayo si ya jumla kutoka kwa wizara ya afya, wahudumu wa afya walikuwa asilimia ishirini na nane ya wale waliopashwa dozi ya kwanza ya chanjo. Kufikia tarehe kumi na tano mwezi wa Aprili asilimia hiyo ilishuka hadi asilimia ishirini na mbili na kufikia tarehe kumi na tisa ya mwezi huo huo ilishuka hadi asilimia kumi na saba, mwishowe ikaja hadi asilimia kumi na saba tarehe mbili mwezi wa Juni. Ilipofikia kwa dozi ya pili, idadi ya wahudumu wa afya ilipanda hadi asilimia themanini na sita ya wale waliopashwa dozi kufikia tarehe mbili mwezi wa Juni mwaka huu. 

Swali ni je ni kwa nini wahudumu wa afya walikuwa na kusuasua kwa kupashwa chanjo…? Katika harakati zangu za udadisi nilizungumza na Daktari Kanyiri, daktari wa umri mdogo anayefanya kazi kwenye kituo cha kibinafsi mji wa Nyeri. Kulingana na Daktari Kanyiri alikuwa na hamu ya kupashwa chanjo tangu kuwasili kwake nchini.

Lakini aliona kuwa wahudumu wenzake walikuwa na kusuasua kwa kupashwa chanjo hizo. Daktari Kanyiri anadai walishawishiwa na picha zenye vidokezo vya kutishia zilizowekwa kwenye mtandao wa Whatsapp, zikionyesha vifo vilivyosababishwa na kupashwa kwa chanjo dhidi ya Covid-19 kutoka sehemu mbali mbali duniani. 

Alafu kukazuka video za kukataa chanjo kutoka kwa wataalam wa madawa.  Moja wapo ikiwa video ya mahojiano ya Daktari Wahome Ngare, daktari wa matibabu ya wanawake ambaye pia ni katibu msaidizi wa chama cha KCD. Mahojiano hayo yalifanywa na Gerald Bitok aliye na wafuasi elfu saba nukta sita kwenye mtandao wa YouTube. Kwenye video hiyo ambayo imeangaliwa na watu elfu kumi tangu kuchapishwa kwake tarehe kumi ya mwezi wa Machi mwaka huu. Daktari Wahome anasisitiza, “Hakuna haja ya chanjo kwani kuna matibabu ambayo yana ufanisi.” Anasema pia hakuna haja ya watu kuzingatia historia ya kimatibabu ili kujua kama watu wanaweza kupata huduma au kusafiri. Jumbe harubaini na nane kwenye video hiyo zinaonyesha kuungwa mkono kwa Daktari Wahome na kauli zake kuhusiana na swala hili. Ni mtumizi mmoja tu alikinzana na msimamo wa Daktari huyu. Kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook video hii imetazamwa mara elfu tisa nukta mbili, kupata jumbe mia mbili sabini na tano na kusambazwa mara mia moja hamsini na tisa. 

Video ya pili ilikuwa ya Daktari Jack Githae, mtaalam wa madawa ya kienyeji anayedai kuwa mshauri wa mashirika mbali mbali kama Shirika la Afya la Dunia na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na mengineo. Video hii imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook ambapo imetazamwa mara elfu tano nukta mbili tangu kupostiwa kwake tarehe kumi na saba Machi mwaka huu, na kwenye mtandao wa YouTube ambako imepostiwa na watumizi wawili tofauti, ambapo imetazamwa na watu mia tano hamsini na nne tangu kupostiwa kwake tarehe kumi na nane mwezi Machi mwaka huu na mia moja thelathini na nne kwa ukurasa wa mtumizi mwingine tangu tarehe ishirini na sita Machi mwaka huu. Katika video hii Daktari Githae anasema serikali isijaribu kupeana chanjo hadi iwe na uhakika wa kutosha wa usalama wa chanjo hizo. Huku akidai kuwa watu kutoka nchi zingine wamekufa ghafla baada ya kupashwa chanjo, anatusihi tusubiri kuona ushahidi wa usalama wake kabla ya kupashwa chanjo hizo. 

Hii ndio njia anayoieleza Daktari Kanyiri, “Waliokuwa na kusuasua waliwachunguza waliopewa dozi yao ya kwanza, na baada ya wiki nne walipoona haina athari zozote ndipo walipo pashwa chanjo,” ananieleza. Wale amabao hawajapata dozi yao ya pili ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe, wanasubiri kwa hamu kwa dozi zingine kuwasili nchini.

Kufikia tarehe tatu Juni mwaka huu dozi bilioni mbili za ugonjwa wa Covid-19 zilipeanwa duniani. Imeripotiwa kuwa kuna nchi kama Izraeli ambazo zimeripoti kupunguwa kwa visa vipya vya maambukizi ya SARS-CoV-2 baada ya idadi kubwa ya watu katika nchi hizo kudungwa sindano mbili za chanjo. 

Kutokana na kusambaa kwa video hizi na athari zake kwa wananchi wa Kenya, nilitumia mbinu ya uchinguzi ya Chanzo cha wazi (Open-Source) kugundua ni nini haswa kinachoshinikiza kampeini za kukataa kupashwa chanjo kwa wataalam wa madawa hawa wawili. 

Dakatari Wahome Ngare anaeleza kuwa chama cha KCDA ni muungano wa madaktari walioamua kufanya kazi yao kwa kuzingatia kanuni za dini ya Kikatholiki. Anadai kuwa matibabu ya kisayansi yanaweza kutumiwa kwa njia isiyo ya sawa na kwamba wataalam wa madawa lazima waweke misingi ya kimaadili. Anasema kuwa chama cha KCDA hakikutoa sababu za kimaadili za msimamo wake wakukataa kupashwa chanjo, bali, wanadai kuwa haina haja kwa sababu kuna njia zenye ufanisi za kimatibabu za kutibu ugonjwa wa Covid-19. 

Katika mahojiano ya televisheni yaliyofanyika mwezi wa Oktoba mwaka wa elfu mbili na kumi na tisa, alitoa madai hayo hayo kuhusu chanjo ya ugonjwa wa HPV, akidai kuwa, “Ni chanjo isiyokuwa na maana na wala hatuihitaji. Chanjo hii kulingana na Kituo cha Kudhibiti magonjwa imesemekana kusaidia kuzuia saratani ya kizazi. 

Miezi isiyopita miwili baada ya chama cha KCDA kutoa kauli kuwa hakuna haja ya chanjo kwa sababu kuna matibabu yenye ufanisi dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, Kiongozi wao Daktari Stephen Karanja alikufa kutokana na ugonjwa huo. 

Chama cha KCDA bado hakijatoa kauli kutokana na kisa hiki, na vile vile hawajaeleza kama bado wako na msimamo huo huo kuhusiana na kupashwa chanjo dhidi ya Covid-19. 

Kuhusiana na video ya pili ya Daktari Jack Githae, ripoti kutoka kwa mtandao inaonyesha kuwa yeye ni daktari wa wanyama aliyesomea udaktari huo Chuo kikuu cha New Mexico, lakini alikuwa na ari ya kusomea dawa za kienyeji, aliyojifundisha kutoka kwa nyanyake mzazi. Alibadilisha mwenendo na kuwa mtaalam kamili wa dawa za kienyeji. Kufikia kwa wakati wa kuchapishwa kwa video yake madai kuwa chanjo zinasababisha vifo yalikuwa yametupiliwa mbali pamoja na madai yake kuwa chanjo hii imeletwa kupunguza idadi ya watu barani Africa. 

Video hizi zinawezakuwa zilichangia kusuasua kwa Daktari Kanyiri kudungwa sindano ya chanjo hapo awali, hofu yake pamoja na ya wenzake ilikwisha walipoona kuwa haina athari zozote mbaya. Anaongeza kuwa anahamu ya kudungwa sindano yake ya dozi ya pili. 

Hivi Punde: Nilimfuatilia Daktari Kanyiri akanieleza anafuraha kwani alidungwa dozi yake ya pili tarehe saba mwezi wa Juni mwaka huu. 

This is an edited and translated version of a story by Jacqueline Wahome which originally appeared here.