19th Ave New York, NY 95822, USA

Kampeini za kupinga kupashwa chanjo au kudungwa sindano kwenye mitandao ya kijamii

By Jael Mboga| August 23, 2021

Maelezo ya Mhariri

Kampeini dhidi ya kupeanwa kwa chanjo zimekuwepo kwa njia moja au nyingine tangu karne ya kumi na tisa. Hivi karibuni kampeini hizi zimeongezeka  haswa  kwenye mitandao ya kijamii. Hii leo kampeini hizi zimeleta pamoja makundi ya watu ambao katu hawangepatana. Makundi haya ni kama, Upande wa kushoto na wa kulia wa kisiasa pamoja na watu wa dini na madhehebu mbali mbali hata wale wasioamini; wakikusanyika kwenye mitandao ya kijamii kusema kuwa chanjo imeletwa na wazungu kuzia muongezeko wa idadi ya wa Aafrika duniani. Chanjo zaidi ya bilioni nne zimepeanwa kimataifa nyingi zikipeanwa katika nchi zinazojiweza, lakini kusuasua bado kuko katika nchi kadha wa kadha ulimwenguni. 

Kampeini za kukataa kupeanwa kwa chanjo katika mitandao ya kijamii zimehitilafiana na jitihada za serikali kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Corona. 

Wakaazi kutoka jiji la Nairobi wanakubaliana na ripoti kuwa jumbe zinazowekwa kwenye mitandao ya kijamii zimeshawishi maamuzi yao kuhusiana na kuchukua au kukataa kwa chanjo dhidi ya ugonjwa huu. 

Wengineo wanadai kuwa ukosefu wa ufahamu uliongezwa na wanaopinga kuwepo kwa ugonjwa huu kama Daktari Stephen Karanja.

 

Tarehe tano mwezi Machi Daktari Karanja alinakiliwa na Kituo cha habari cha Nation akisema, “Kuna uwekezaji ambao Bill Gates ameufanya na unahitaji dunia nzima kupewa chanjo. Swala nyeti ni je, uwekezaji huo ni upi…?”

Daktari Karanja alieneza habari potovu kuhusu chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona na baadaye akafa kutokana na ugonjwa huo. 

Mwanabiashara Evelyn Moraa anasema kuwa ni vigumu kupuuza jumbe nyingine zinazowekwa kwenye mitandao ya kijamii. 

Moraa aliuliza, “Ni vipi dalili za virusi vinavyo sababisha maafa ni moja wapo ya dalili za magonjwa mengine mengi…?” Moraa akiwa anamaanisha, kuumwa na kichwa na kudondokwa na makamasi. 

Hofu kubwa kwa Moraa ikiwa shida ya kupata mtoto baada ya kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa huu. 

Vile vile Martin Koss aliweka jumbe hii kwenye mtandao, “Tunaelezwa kuvaa barakoa, tufanye usambazaji wa kijamii, tusiwe na mikusanyiko ya watu kana kwamba tuko na virusi hivi.

Watoto wetu wanawekewa mipaka na bado tunaambiwa tufunge biashara zetu…Hii ni njia ya kuharibu maisha yetu.”

Beatrice Mmboga mwanamke wa miaka thelathini na nane na mama wa watoto wanne anakubaliana na Bwana Koss. 

Huku akisema hata kama ana watoto wanne tayari hangependa kuchukua chanjo ambayo itamzuia kupata watoto zaidi baadaye.  

“Mama yangu mzazi alikuwa na watoto watano iweje mimi nipate kidogo kuliko hao,” Anatueleza akicheka. 

Utafiti wa habari kwenye mtandao wa Twitter unaonyesha wengi wanaokataa chanjo mitandaoni wanaamini kuwa vyombo vya habari vime ongeza chumvi habari kuhusiana na janga la Corona na kwamba ugonjwa wa Covid-19 ni nadharia ya njama. 

Mtumizi mmoja anakwenda kwa jina la, “Sitaki chanjo nisiyo hitaji,” kwenye ‘handle’ ya @AmAntiVaxism.

A Twitter account “l Don't Want A Vaccine I Don't Need” under the handle @iAmAntiVaxism.
A Twitter account “l Don’t Want A Vaccine I Don’t Need” under the handle @iAmAntiVaxism.

 

Ni vigumu kubainisha kama ni mwanamke au mwanamume. Habari kwenye ukurasa wake inaeleza kuwa picha tunayoiona siyo ya anayekarabati akaunti hii. Mtumizi huyu anaongeza #Refusnik ikimaanisha mtu aliyekataa kufuata maagizoama kutii sheria kama njia ya kupinga jambo fulani. 

Jumbe ya Mtumizi huyu inasema, “Mimi sio mnadharia wa njama. Mimi ni mtu anayefikiria kwa kina na siamini chochote kinachoelezwa na vyombo vya habari.”

Fulana yake imeandikwa, Tayari kwa wikendi ijayo #26 Juni 2021 #tuungane kwa uhuru #Mimi si panya wa majaribio kwenye maabara #Nakubaliana na maamuzi yakibinafsi #Nakataa paspoti za kusafiria kwa wenyekupashwa chanjo pekee #Sidungwi sindano katu. Juni, 17, 2021.

Mtumizi mwingine kwa jina la Mama wa Tumaini alikosoa makala yaliyochapishwa kwenye BBC yaliyo eleza uhusiano kati ya dalili za kuumwa na kichwa na kudondokwa na makamasi kwa aina ya kirusi cha Corona cha Delta Variant. 

Akieleza, “Jinsi ya kushawishi uwepo wa janga la Corona kupitia kwa dalili mbili za kawaida kwa ugonjwa mwingine wowote tangu historia ya dunia… “Kuumwa na kichwa na kudondokwa na makamasi kwa husishwa na aina ya kirusi cha Delta Variant.”

Twitter Post
Twitter Post

 

BBC tarehe kumi na nne mwezi wa Juni ilichapisha kuwa, kuumwa na kichwa, maumivu ya koo na kudondokwa na makamasi ndizo dalili tatu kuu zinazohusishwa na ugonjwa wa Corona Uingereza. 

Tim Spectro ambaye ni kiongozi-mwelekezi wa kituo cha kuangalia dalili za ugonjwa wa Covid-19 cha Zoe alieleza kuwa aina ya kirusi cha Delta kinaweza kuhisi kama homa mbaya ya mafua haswa kwa vijana. 

Shirika la Afya Ulimwenguni limeorodesha dalili za ugonjwa wa Corona kuwa, homa, kukohoa na ukosefu wa pumzi. Huku visa vibaya zaidi vikisababisha ugonjwa wa nimonia na shida za kupumua. 

Shirika hilo limeorodhesha homa, kikohozi kikavu na kuchoka kama dalili zilizoshuhudiwa kwa wagonjwa wengi. 

Nazo dalili zilizoshuhudiwa kwa wagonjwa wachache zikiwa maumivu ya mwili, maumivu ya koo, kuharisha, kiwambo, kuumwa na kichwa, kukosa  ladha au kupoteza uwezo wa kunusa, harara na kubadilika kwa rangi kwenye vidole na miguu.

Dalili hatari zaidi ikiwa ukosefu wa pumzi, au kupungukiwa kwa pumzi, maumivu au shinikizo kwenye kifua, kushindwa kuzungumza au kutembea. 

Kumekuwepo na wito wakuchukua hatua za kisheria kwa watu wanaoeneza habari potovu kuhusu kupeanwa kwa chanjo kwenye mitandao ya kijamii .

Huku wengine wakidai kufanya hivyo kutakwenda kinyume na sheria iyo hiyo huku wakishauri badala yake kuelimishwa kwa uma na Serikali kuhusu kupeanwa kwa chanjo.

Huku jumbe nyingine kama ya Moraa kwenye mitandao ya kijamii ikiwa kuwa wengi wanao pinga chanjo hizo hawana habari zakutosha kuzihusu. 

“Serikali yenyewe haiwezi kutupa habari zaidi kuhusiana na chanjo hizo kupeenwa kwa wanawake wajaa wazito ama athari zake kwa watu wanaotaka kupata watoto siku zijazo. Hata kama wanasema ziko salama kwa matumizi lazima kuna athari zinazotokana na chanjo hizo. Hivyo basi watujulishe athari hizo ni zipi…?” Alieleza. 

Mtumizi mmoja kwa jina la Erdocon alisema, “Kuna masawala kuhusiana na athari za chanjo hii ambayo ni lazima yashughulikiwe. Haipaswi kupuuza kila swala. Mawazo yangu ni kuwa mjadala kuhusiana na athari na faida za chanjo hizi ni muhimu ufanywe.”

Akiwa na ujaa uzito wakati huu wa Corona, Priscila Nyaboke ametulia kwenye saluni yake kwenye eneo la makaazi duni ya mabanda la Mlango Kubwa akiwasubiri wateja. 

Nyaboke anakula tambi alizozipakia kwenye dishi ya chakula cha mchana akiwa amewekeza dishi hiyo kwenye tumbo lake lilombeba mtoto. 

Ananieleza kuwa anashauku kama madaktari wanaelewa ugojwa wa Corona na hivyo basi hana imani na chanjo ya OXFORD/AstraZeneca ambayo inatumiwa nchini hivi sasa.

Oxford/AstraZeneca vaccine
Oxford/AstraZeneca vaccine

 

Kama wengi katika hali yake Nyaboke anawasiwasi kuwa na uja uzito wakati wa janga hili. 

Takriban zaidi ya dozi milioni moja za chanjo ya Oxford/AstraZeneca ziliwasili nchini kwenye uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mwezi wa Machi tarehe tatu. 

Serikali ikiongozwa na waziri wa Afya Mutahi Kagwe,  iliwarai wananchi kwenda na kupewa chanjo. 

Kile ambacho serikali haikutarajia ni habari potovu zilizohusishwa na chanjo hizo na athari ya habari hizo kwa zoezi la kupeanwa kwa chanjo hizo. 

Moja wapo ya habari hizo potovu ni kwamba chanjo hizo zinaweza kumuathiri kijusi  na kuathirisha kizazi na kupata mtoto kwa anayezichukua.

Nyaboke aliye na miaka ishirini na mbili. Ananieleza kuwa anahofu ya kuatharisha mimba yake ya kwanza na kuwa angetaka kupata watoto zaidi baadaye. 

“Kwa sasa mimi ndio mzazi pekee wa mtoto huyu baada ya mpenzi wangu kukataa mimba yangu kwa hivyo kukiwa na shida yoyote hakuna mtu wakunisaidia, niko peke yangu.” 

Nyaboke ameilaumu serikali kwa kile amekiita ukosefu wa habari za kutosha, kuhusiana na athari za virusi hivyo kwa wamama wajaa wazito, wamama waliojifungua watoto na wale wanaotaka kupata watoto siku zijazo. 

Katika hotuba za kila siku kuhusiana na ugonjwa wa Corona kwa wanahabari, afisa mkuu wa utawala katika wizara ya Afya Daktari Mercy Mwangangi aliripoti kuwa idadi ya watu wanaoenda hospitali imepungua ikiwa ni pamoja na wanawake wajaa wazito. 

Wakenya wengi wanaohitaji huduma za kimatibabu wakikosa kwenda hospitali kwa hofu ya kuumbukizwa ugonjwa wa Corona. Huku Daktari Mwangangi akiwarai wananchi waende kupata matibabu wanapo yahitaji.

Hospitali ya Agakhan hapa Nairobi imechapisha kwenye tovuti yake kwamba chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona hazipeanwi kwa wingi kwa wamama wajaa wazito kwani majaribio katika maabara hayaonyeshi athari zozote kwa mama au mtoto. 

Anaongeza akisema, “Umuhimu haswa ya majaribio kwa wanyama ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona bado haijabainishwa. Kupeanwa kwa chanjo ya Oxford/ AstraZeneca kwa wamama wajaa wazito kunafaa wakati kumebainika kuwa manufaa ya chanjo hiyo yanazidi athari kwa mama au mtoto.”

Kauli hii ikizidisha wasiwasi wa Nyaboke kuhusiana na kupokea  chanjo hii. Nyaboke bado hajapokea chanjo na hana mpango wa kupokea chanjo yoyote.

Tovuti ya hospitali ya Agakhan pia inaeleza kuwa kuna ushahidi kuwa kuna aina ya chanjo ambayo ikipeanwa kwa mama anayenyonyesha mtoto anaweza kupata kiwango cha ulinzi. 

Hofu ya Nyaboke iliongezwa na ripoti iliyochapishwa Kwenye Business Daily mwezi wa Aprili iliyosema, “Majaribio yaliyofanywa mwanzoni hayakuzingatia wamama wajaa wazito na wanaonyonyesha. Majaribio yanayo angalia jinsi chanjo hizo zinavyofanya kazi kwa wamama wajaa wazito na kwa wanaonyonyesha bado hayajakamilishwa.”

Kenya Conference of Catholic Bishops' Dr Stephen Karanja in Nairobi on 28/07/2015. He was against the distribution of the Covid-19 vaccine. He died of Covid-19 on April 29. [File, Standard]
Kenya Conference of Catholic Bishops’ Dr Stephen Karanja in Nairobi on 28/07/2015. He was against the distribution of the Covid-19 vaccine. He died of Covid-19 on April 29. [File, Standard]

Ripoti hiyo ikiongeza kuwa majaribio hayo hayakufanyiwa kwa wanawake wajaa wazito.

“Data kuhusiana na athari za chanjo hizi kwa wamama wajaa wazito haitoshi. Hata hivyo idadi chache ya wanawake waliofanyiwa majaribio hayo walipata uja uzito baada ya zoezi hilo.” Ripoti hiyo ilisema. 

Tulipoendelea kujadiliana na Nyaboke alitueleza kwamba kukataa kwake kwa chanjo kumeongezwa na kauli za Kiongozi wa Chama cha Madaktari Wakatholiki, Daktari Stephen Karanja. 

Huku akisema kuwa maoni ya Mtaalam hayawezi kupuuzwa na, “Watu wa kawaida kama mimi.”

Mwezi wa Machi mwaka huu kanisa la Katholiki lilipata upinzani mkali kutoka kwa Chama cha Madaktari, kanisa hilo lilipoeneza habari za uwongo kuhusiana na chanjo za Covid-19. 

Mwezi uliopita  Madaktari wa kanisa la Katholiki walisema hakuna haja ya wakenya kupokea chanjo. 

Daktrai Karanja alipinga kusambazwa na kupeanwa kwa Chanjo dhidi ya Covid-19. 

Maoni haya yakija siku chache baada ya maoni aliyoyatoa tarehe tatu mwezi wa Machi yaliyosema, “Kuacha uharibifu na kupotea kwa maisha kunako sababishwa na maradhi ya Covid-19.”

Maoni haya yaliyowekwa kwenye waraka wa kurasa tisa yalifwatwa na mengine mengi kama, nadharia ya kudhibitiwa kwa idadi ya watu na madai kuhusiana na kupimwa na kutibiwa kwa ugonjwa wa Corona. 

Kulingana na AFP inayobainisha ukweli, kati ya mapendekezo aliyoyapendekeza Daktari Karanja ya kutibu ugonjwa wa Corona ni kama, kuvuta pumzi ya mvuke mara kadhaa kwa siku, kunywa tembe za Ivermectin na kufuata itifaki za Zelenko zinazohusisha kuchukua mchanganyiko wa dawa kila siku kwa wiki. 

Itifaki ya Zelenko iko na mchanganyiko wa dawa kama hydroxychloroquine, Zinc na Azithromycin (antibiotiki) ambazo unachukua kwa siku saba. 

Wataalam wa kimatibabu wanasema mbinu hizi hazijabainika kufanya kazi. 

Tarehe 29 mwezi wa Aprili Daktari Karanja alikufa kutokana na maradhi ya Covid-19. Alifariki katika hospitali ya Mater alipokuwa amelazwa  kwenye kitengo chenye utegemezi mkubwa. 

Ujumbe ulioonekana kutoka kwa mfanyikazi mwenzake Daktari Wahome Ngare na vyombo vya habari vya The Standard, tarehe ishirini Aprili ulisema alikufa kutokana na shida zinazosababishwa na ugonjwa wa Covid-19. 

Kwa wakati huu Nyaboke amesema hatapashwa chanjo hadi atakapo pata habari zaidi kuhusiana na athari za chanjo hiyo kwake na kwa kijusi wake. 

This is an edited and translated version of a story by Jael Mboga which originally appeared on The Standard.